Description
Umoja wa Waislamu ni muhimu sana, na wakati huu suala hili linazidi kuwa na umuhimu mno. Tangu zamani kumekuwepo kutokuelewana kusiko kuwa na maana kati ya madhehebu mbili kubwa za Kiislamu – Sunni na Shia. Katika baadhi ya sehemu hali hii mbaya ilishadidi kiasi cha kufikia wafuasi wa kila madhehebu kuona kwamba ni halali kumwaga damu ya mfuasi wa madhehebu nyingine.
Hali hii haipwasi kuachwa iendelee, lazima wajitokeze viongozi wa kila madhehebu kulikemea na kulitafutia ufumbuzi. Kwa hakika wako viongozi katika kila upande ambao huutakia mema Uislamu wetu, ambao hawataki malumbano juu ya hitilafu zilizopo kati ya madhehebu zao. Kwao hitilafu hizo ni ndogo sana na kwamba mambo ambayo yanawaunganisha ni mengi zaidi ambayo ndiyo mambo ya msingi katika Uislamu, kinyume na yale machache wanayohitalifiana ambayo sio ya msingi katika Uislamu. Mathalan, wote wanakubaliana katika misingi mikuu mitatu ya Uislamu – Tawhidi, Utume na Kiyama. Wote wanasali sala tano za kila siku, wote wanafunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, wote wanatoa zaka, wote wanakwenda kuhiji, wote wanaposali huelekea Kaaba, wote wanasoma Qur’ani moja, wote Mtume wao ni mmoja Muhammad (s.a.w.), na kwamba wote wanaamini kwamba Muhammad ni Mtume wa mwisho hatakuja Mtume mwingine baada yake, wa mwanzo wao akiwa ni Nabii Adam (a.s.). Haya ni machache katika mengi wanayokubaliana. Hivyo viongozi wa kidini kwa busara zao huaangalia yale tu mengi yanayowaunganisha na kujishughulisha nayo na kuachana na yale machache ambayo huhitalifiana ili kuleta mkuruba na umoja katika Uislamu.